Washukiwa tisa wanaohusishwa na moto uliotokea katika Shule ya wasichana ya Utumishi na kusababisha vifo vya wanafunzi 16 wataendelea tena kusalia rumande wakisubiri hatima yao siku ya Jumatano, Juni 3, Citizen imeripoti.

Wakifika mbele ya Hakimu Mkuu wa Naivasha, Abdulqadir Ramathan, upande wa mashtaka uliomba kuongezewa muda wa siku 30 wa kuwashikilia washukiwa hao ili kukamilisha uchunguzi.

Ingawa ombi hilo lilipata uungwaji mkono kutoka kwa mawakili wanaowawakilisha waathiriwa, lilipingwa na mawakili wa washukiwa hao.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa sababu zilizotolewa za kuendelea kuwazuilia washukiwa hazikuwa na uzito wa kutosha.

Hatua ya mahakama kuhusu ombi hilo inatarajiwa kutolewa Jumatano, Juni 3.

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkuu Abdulqadir Ramathan alisema kuwa mahakama itatoa uamuzi kesho mchana kuhusu iwapo washukiwa wataachiliwa kwa dhamana ya fedha au kama upande wa mashtaka utaruhusiwa kuwaweka rumande kwa siku 30 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Haya yanajiri baada ya washukiwa hao kuwaeleza wachunguzi sababu zilizowasukuma kutekeleza kitendo hicho.

Kwa mujibu wa maelezo yao, walikuwa wakipinga mabadiliko yaliyofanywa kwenye ratiba ya mitihani, uamuzi wa shule kuwatoza ada kwa ajili ya shughuli ya kitamaduni, pamoja na ushawishi kutoka kwa wenzao kufuatia mgomo uliotokea katika shule jirani ya wavulana.

Washukiwa hao walidai kuwa mpango wa kuchoma bweni hilo ulipangwa saa tatu usiku (9:00 p.m.) na kutekelezwa saa sita usiku (12:00 a.m.), takribani saa tatu baadaye