Rais wa Ghana, John Mahama, amesema kuwa muswada mpya unaolenga kuhalalisha adhabu kali dhidi ya shughuli za LGBTQ+ utapitia uchunguzi wa kisheria kabla ya kuidhinishwa rasmi.

Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Uingereza, Mahama alisema kuwa mshauri wake wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali watauchunguza muswada huo kwa sababu ulikuwa umeletwa bungeni kama muswada wa wabunge binafsi, si muswada wa serikali.

Muswada huo, uliopitishwa na Bunge la Ghana siku ya Ijumaa, unapendekeza kifungo cha hadi miaka mitatu kwa mtu anayejitambulisha kama mwenye mahusiano ya jinsi moja na mwenye jinsia mbili (bisexual), mwenye utambulisho wa kijinsia tofauti (transgender). Pia unapendekeza kuwepo kwa “wajibu wa kuripoti” vitendo vinavyopigwa marufuku kwa polisi.

Mahama alisema:

“Tutauangalia na kuhakikisha kuwa kila kitu kiko sawa.”

Aliongeza kuwa ikiwa kutakuwa na matatizo yoyote ya kisheria au kiutaratibu, muswada huo utapelekwa kwa Baraza la Taifa (Council of State), ambalo ni chombo chake cha ushauri.

Tangu aingie madarakani mwaka jana, Mahama amekuwa akishinikizwa na viongozi wa dini kuimarisha sheria zinazopinga mapenzi ya jinsi moja.

Kwa sasa, mahusiano ya jinsi moja tayari ni kinyume cha sheria nchini Ghana chini ya sheria zilizoanzishwa wakati wa ukoloni wa Waingereza.

Katika kikao cha maswali na majibu jijini London siku ya Jumatatu, Mahama pia alisema kulikuwa na mapungufu ya kiutaratibu wakati wa kupitishwa kwa muswada huo, na kwamba Spika wa Bunge anashughulikia suala hilo.

Hii ni mara ya pili kwa wabunge wa Ghana kuunga mkono sheria ya aina hiyo. Muswada unaofanana ulianzishwa kwa mara ya kwanza bungeni mwezi Agosti 2021 baada ya kituo cha rasilimali za LGBTQ+ kufungwa katika mji mkuu wa Accra.

Muswada huo umezua mjadala mkubwa ndani na nje ya Ghana, huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakieleza wasiwasi kuhusu athari zake kwa haki za msingi na uhuru wa watu wa LGBTQ+.