Serikali imeagiza Jeshi la Polisi pamoja na Madawati ya Jinsia nchini kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vinavyokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na ushoga, ukahaba na uendeshaji wa madanguro.


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alipokuwa akizungumza Bungeni, ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16, inayobainisha makosa mbalimbali ya jinai yanayohusiana na makosa ya kijinsia na uendeshaji wa biashara haramu za ngono.

Amesema vifungu vya 139 hadi 147 vya sheria hiyo vinaeleza wazi makosa yanayohusiana na vitendo hivyo, na kwamba mamlaka husika zitaendelea kuchukua hatua mara pale ushahidi wa kutosha utakapopatikana.

Aidha, Waziri Katambi ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na uendeshaji wa madanguro na shughuli za ukahaba, akibainisha kuwa sheria inakataza kumiliki au kunufaika na mapato yatokanayo na biashara hiyo pamoja na kushiriki kwa namna yoyote ile.

Kwa upande wake, Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga, alihoji kauli ya Serikali kuhusu kuongezeka kwa matukio ya vitendo vya ushoga katika baadhi ya maeneo ya makazi, akidai kuwa hali hiyo imeanza kujitokeza katika baadhi ya kata na mitaa licha ya uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alieleza kuwa vitendo vya ushoga ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania, na wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.

Amesema mchakato wa kushughulikia makosa hayo unahusisha uthibitishaji wa tuhuma, uchunguzi wa kina, upelelezi wa kina wa vyombo vya dola, na hatimaye kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa taratibu za sheria.

KATAMBI amesitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wahalifu wote wanaobainika kutenda makosa ya jinai wanachukuliwa hatua sawa na wengine wote bila upendeleo, kwa mujibu wa sheria za nchi.