Abiria mmoja ameripotiwa kukaribia kuvutwa nje kupitia dirisha la ndege akiwa angani katika ndege ya Ryanair.
Mashahidi waliambia vyombo vya habari vya eneo hilo kwamba mwanaume huyo, anayesemekana kuwa raia wa Serbia mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, alining'inia nje ya dirisha akiwa ametanguliza kichwa hadi kufikia mabegani kwa dakika kadhaa, kabla ya abiria wengine waliokuwa kwenye ndege kufanikiwa kumvuta na kumrudisha ndani.
Katika taarifa yake, kampuni ya Ryanair ilisema kuwa ndege yake ya Ijumaa asubuhi kutoka mji wa Thessaloniki nchini Ugiriki kuelekea Memmingen nchini Ujerumani ilirejea muda mfupi baada ya kupaa, baada ya dirisha la abiria kulegea na kutoka kwenye sehemu yake wakati ndege ikiwa angani.
Taarifa hiyo iliendelea kusema: "Ndege ilitua salama kama ilivyopangwa, na abiria kurejea kwenye eneo la kusubiri ndege. Abiria mmoja aliomba na kupatiwa huduma ya matibabu akiwa uwanjani Thessaloniki."
Shirika la ndege la gharama nafuu la Ireland, Ryanair, liliongeza kuwa "ndege mbadala iliandaliwa ili kuwapeleka abiria hadi Memmingen" saa kadhaa baadaye.
Ripoti za vyombo vya habari nchini Ugiriki na Ujerumani ziliwanukuu baadhi ya abiria wakieleza kuwa walisikia mlio mkubwa wa kishindo, kisha dirisha likapasuka na barakoa za oksijeni zikadondoka kutoka kwenye dari ya ndege muda mfupi baada ya ndege aina ya Boeing 737 kupaa.
Inaaminika kuwa dirisha hilo lilivunjwa na vipande vilivyotoka kwenye injini ya ndege, ingawa Ryanair haijatoa maoni kuhusu madai hayo.
"Tuligundua mara moja kwamba kulikuwa na upotevu wa shinikizo la hewa ndani ya ndege. Kulikuwa na mayowe... kwa muda mfupi nilidhani mtu alikuwa amefungua kwa bahati mbaya mlango wa dharura," alisema Christina, mmoja wa abiria, katika mahojiano na Radio Thessaloniki.
0 Comments