Jeshi la Nigeria limesema wanajeshi wa Kikosi cha 3 cha Operesheni ya Pamoja inayoendelea Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo, wamefanikiwa kumkamata raia wa kigeni anayeshukiwa kusambaza dawa za kulevya na pombe kwa wapiganaji wa Boko Haram.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Nigeria, Mohammed Goni, operesheni hiyo ilifanyika baada ya kupokea taarifa za kijasusi zilizowasaidia kumfuatilia mshukiwa huyo.

Mwanamke huyo alikamatwa hapo jana, Julai 9, akiwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya, pombe na bidhaa nyingine haramu zilizodaiwa kuwa zilikuwa zikipelekwa kwa wapiganaji wa Boko Haram.

Mshukiwa ametambulika kwa jina Rachael Samuel, mwenye umri wa miaka 48, kutoka Chad.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Samuel alikuwa akisafirisha bidhaa hizo kuelekea maeneo ya visiwa vya Ziwa Chad ambavyo vinajulikana kuwa maficho ya makundi ya kigaidi.

Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni mifuko saba ya bangi, pombe na bidhaa nyingine zinazodaiwa kusafirishwa kwa ajili ya wapiganaji wa Boko Haram..