Waziri wa Utamaduni wa Israel, Miki Zohar, ametoa wito wa kuwapokonya uraia watayarishaji wa filamu ya “Naza”, inayozungumzia vifo vya raia wa Gaza, akiwashutumu kwa “uhaini.”

Watayarishaji wa filamu hiyo, Rachel Zar na Yuval Abraham, walielezea kuwa filamu hiyo ya Naza inaakisi kipindi cha giza eneo la Gaza.

Filamu hiyo, iliyotengenezwa kwa ushirikiano na gazeti la The Guardian, inajumuisha ushahidi kutoka kwa mashuhuda 24 kutoka jeshi na idara za ujasusi za Israel, wanaodai kuwa mifumo inayotumia akili mnemba ilitumika katika mashambulizi dhidi ya Gaza, na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya watu.

Filamu hiyo yenye urefu wa dakika 80 ilitunukiwa tuzo maalum katika Tamasha la Filamu la Venice, huku ikishangiliwa kwa makofi na vifijo kwa dakika 25 ilipoonyeshwa kwa mara ya kwanza.

Mmoja wa vyanzo vilivyozungumza katika filamu hiyo,alidai kuwa amri ilitolewa ya kuuawa kwa raia 500, ili kumlenga mwanachama mmoja wa Hamas.

Waziri Zohar aliwashutumu watayarishaji wa filamu hiyo kwa kuidhuru Israel ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa “makundi yanayowachukia Wayahudi”.

Jeshi la Israel awali lilikataa madai yaliyoonyeshwa katika filamu hiyo, likipinga matumizi ya ushahidi kutoka kwa watu ambao hawakutajwa majina. Hata hivyo, baadaye lilisema madai hayo yanapaswa kuchunguzwa kwa kina na kuthibitishwa kwa ushahidi.