Zaidi ya watu 2,000 wamekimbia kutoka Yemen hadi nchini Djibouti, baada ya mapigano kati ya kundi la Wahouthi na majeshi ya serikali ya Yemen kuongezeka.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa, mapigano mapya nchini Yemen yamesababisha watu 85,818 kuyahama makazi yao kufikia sasa.

Waasi wa Houthi waliteka mji wa bandari wa Mocha kwenye Bahari ya Shamu siku ya Alhamisi wiki iliyopita, na tangu wakati huo wameendelea kudhibiti maeneo ya pwani na visiwa vinavyozunguka Mlango wa Bab al-Mandeb.

Mashambulizi hayo yamewalazimisha maelfu ya familia kukimbia makazi yao, huku ripoti zikisema vijiji vizima katika maeneo ya Maqbanah, Jabal Habashi na al-Maafer vimeachwa bila wakazi.

Mamlaka za Djibouti zimesema zinashirikiana na Jeshi la Wanamaji, Jeshi la nchi kavu, Polisi na wahudumu wa afya, kwa msaada wa IOM na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwashughulikia wakimbizi wanaowasili nchini humo.

Waliowasili, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wamepelekwa katika kituo cha Markazi mjini Obock, ambako wanapatiwa maji chakula.

Idadi ya wakimbizi hao inatarajiwa kuongezea huku mapigano nchini Yemen yakiendelea.