Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kupatiwa taarifa ya uchunguzi kuhusu majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda yaliyotitia, huku akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika iwapo itabainika kuwa kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa mradi huo.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nyamuswa, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

Amesema ameelezwa kuwa tayari Waziri wa Afya alishaunda timu ya uchunguzi na suala hilo pia limefanyiwa kazi na TAKUKURU, hivyo ameitaka taarifa hiyo iwasilishwe ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waliohusika.

Dkt. Mwigulu amesema haikubaliki kwa mtu anayebainika kufanya makosa katika utekelezaji wa mradi mmoja kuhamishiwa eneo jingine na kuendelea na mwenendo huo bila kuwajibishwa.

Katika ukaguzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema amekuta majengo mawili yakiwa yametitia na kupewa maelezo kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa maji katika eneo la mradi pamoja na udongo wa mfinyanzi.

Amehoji sababu hizo, akitaka kubainika iwapo mazingira hayo yalikuwepo kabla ya ujenzi kuanza na kwa nini hayakuzingatiwa wakati wa maandalizi na utekelezaji wa mradi.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo hadi ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia ubainike, huku akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kubeba gharama za uzembe katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

HATUA ZA KUPUNGUZA BEI YA SARUJI

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji nchini.

Amesema ameelekeza kuondolewa kwa kodi kwenye klinka, ambayo ni moja ya malighafi muhimu inayotumika katika uzalishaji wa saruji.

Hatua hiyo, amesema, inalenga kuhakikisha upatikanaji wa saruji unakuwa wa uhakika na kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji ili bei iweze kuwa himilivu kwa wananchi.

Serikali pia imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, ili kulinda fedha za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizokusudiwa.