Maelfu ya Wakenya walikusanyika katika maeneo mbalimbali nchini siku ya Ijumaa jioni kuwasha mishumaa kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na kiongozi wa zamani wa ODM, Raila Odinga, maarufu kama ‘Baba’.
Hafla hiyo ya kitaifa iliyofanyika jioni ya tarehe 2 Oktoba ilikuwa sehemu ya kuanza kwa mpango wa mwezi mzima ya kumbukumbu iliyopewa jina la “Mwezi wa Baba”, inayoandaliwa kuelekea kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha Raila tarehe 15 Oktoba 2025.
Mjini Nairobi, mkusanyiko mkuu ulifanyika katika ustani ya Uhuru Park, ambako shughuli zilianza majira ya saa tisa alasiri kabla ya hafla ya kuwasha mishumaa kuanza saa 12 jioni. Waombolezaji na wafuasi wa Raila walifika wakiwa na mishumaa, maua na picha zake.
Shughuli kama hizo pia zilifanyika katika maeneo mengine nchini, yakiwemo Treasury Square mjini Mombasa na Kisumu Central Square. Hafla hizo zilifanyika kwa wakati mmoja saa 12 jioni, kama sehemu ya zoezi la kitaifa lililoandaliwa na chama cha ODM.
Mjini Mombasa, mwanawe Raila, Raila Odinga Junior, alijiunga na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na viongozi wengine katika hafla hiyo ya kumbukumbu.
Nairobi, historia na urithi wa Raila pia vilionyeshwa kwenye mnara wa KICC, uliowashwa kwa picha na ujumbe wa kumuenzi mwanasiasa huyo wakati wa usiku.
Kwa mujibu wa waandaaji, shughuli za kumbukumbu zitaendelea katika maeneo mbalimbali nchini Kenya mwezi mzima wa Oktoba. Miongoni mwa shughuli zilizopangwa ni mikutano ya kumbukumbu katika maeneo tofauti kabla ya shughuli za kilele kuelekea tarehe 15 Oktoba.
Utaratibu huo unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 31 Oktoba kwa tamasha la kitaifa la muziki na kumbukumbu ya urithi wa Raila mjini Nairobi.
Hata hivyo, familia ya Raila na kamati ya kitaifa ya maandalizi ya kumbukumbu pia imepanga shughuli zake. Miongoni mwa hizo ni hafla ya kimataifa ya kuwasha mishumaa tarehe 14 Oktoba huko Kang’o ka Jaramogi, Bondo, siku moja kabla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo chake. Hafla hiyo itaongozwa na mjane wake, Ida Odinga.
0 Comments