Maelfu ya watu katika maeneo mbalimbali ya Hispania wameandamana wakitaka serikali kuimarisha ulinzi wa wapangaji.

Maandamano hayo yameibuka baada ya serikali kushindwa kupitisha sheria ya dharura ya kushughulikia tatizo la makazi.

Takriban maandamano 50 yalifanyika Jumamosi katika miji kadhaa, ikiwemo Madrid, Valencia na Barcelona.

Mapigano pia yalizuka kati ya baadhi ya waandamanaji na polisi.

Maandamano yameenea nchini Hispania baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 87 kufukuzwa katika nyumba aliyokuwa akiishi kwa kushindwa kumudu ongezeko kubwa la kodi ya nyumba.

Picha zilionyesha polisi wakikabiliana na waandamanaji karibu na Palau de les Arts Reina Sofía, ambako mkutano wa sekta ya mali isiyohamishika ulikuwa ukiendelea katika jiji la Valencia, lililoko mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, baadhi ya waandamanaji walirusha vizuizi na vitu mbalimbali dhidi ya polisi, ambao walijibu kwa kutumia risasi za mpira.

Shirika la utangazaji la umma la RTVE liliripoti kuwa maafisa tisa wa polisi walijeruhiwa na watu watano walikamatwa.