Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila, amemshutumu mrithi wake, Felix Tshisekedi, kwa kusaini makubaliano na Marekani kuhusu madini muhimu, akisema alifanya hivyo kwa matumaini ya kupata uungwaji mkono wa Marekani bila masharti, jambo alilolitaja kuwa ni dhana potofu.
Kabila alitoa kauli hiyo jana, hii ni kwa mujibu wa chombo cha habari cha kujitegemea cha Actualite.cd,Katika hotuba yake ya tarehe 9 Oktoba, Kabila alisema kuwa makubaliano ya madini ya aina hiyo hufanywa kati ya mataifa, badala ya tawala za kisiasa, na hivyo hayahakikishi kuendelea kuwepo madarakani kwa serikali husika.
Rais huyo wa zamani aliahidi kutangaza hatua madhubuti zinazolenga “kuiokoa” nchi kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na kiusalama, akionya kuwa kuna matumaini machache ya hali kuboreka chini ya uongozi wa Tshisekedi.
Pia aliwataka wananchi kuchukua jukumu la kuamua mustakabali wa nchi yao, akiahidi kuchukua hatua zaidi katika “saa, siku na wiki zijazo”.
Kauli zake zinatolewa wakati kukiwa na kutokubaliana kuhusu mpango wa Tshisekedi wa kufanya mazungumzo ya kitaifa, uliotangazwa mwezi Agosti kwa lengo la kushughulikia migawanyiko ya kisiasa na ukosefu wa utulivu uliodumu kwa muda mrefu.
Washirika wa kisiasa wa Kabila wamehoji iwapo mazungumzo hayo yaliyopendekezwa yatawashirikisha wadau wote kwa usawa, na kutaka kuwepo kwa dhamana imara zaidi kuhusu maandalizi yake, uratibu na ushiriki wa washiriki.
Mvutano huo wa kisiasa unaendelea huku mapigano yakiendelea mashariki mwa DR Congo kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Muungano wa Mto Congo AFC/M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Marekani na Qatar za kufanikisha amani.

0 Comments