Sagal Abdi-Wali alishinda uchaguzi mdogo wa eneo la Holborn na St Pancras siku ya Alhamisi, na kuwa Mwingereza mwenye asili ya Somalia wa kwanza kuchaguliwa kuwa Mbunge.

Abdi-Wali, mwenye umri wa miaka 42, ambaye alifika Uingereza akitokea Somalia akiwa mtoto mkimbizi pamoja na familia yake katika miaka ya 1990, alikulia Camden, alifanya kazi katika Halmashauri ya Camden kama afisa wa masuala ya makazi na alichaguliwa kuwa diwani mwaka 2022.

Alichukua wadhifa wa kiongozi wa halmashauri hiyo mwezi Mei, na chama cha Labour kilisisitiza sana kuhusu uhusiano wake na eneo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi.

Akizungumza baada ya ushindi wake, Abdi-Wali aliahidi kufanya kazi ili kuboresha maisha ya familia, akiongeza: "Tatizo la ukosefu wa makazi ndilo lililonisukuma kuingia katika siasa."

Kwa mujibu wa chama cha Labour, Abdi-Wali amefanya kazi kama mtu wa kujitolea na mdhamini wa mashirika ya kutoa misaada ya kijamii kwa zaidi ya muongo mmoja, ikiwa ni pamoja na kuhudumu kama mjumbe wa bodi ya shule katika shule mbili, na kama Afisa wa Serikali za Mitaa katika halmashauri hiyo.


Sagal Abdi-Wali awa kiongozi wa Baraza la Camden mwezi Mei

Kabla ya kuwa kiongozi wa halmashauri, alihudumu kama mjumbe wa kamati kuu ya halmashauri hiyo anayeshughulikia masuala ya makazi bora.

Kwa mujibu wa halmashauri hiyo, katika wadhifa huo "alisimamia na kuendeleza juhudi za halmashauri kuhakikisha kuwa watu kote Camden wanaishi katika nyumba salama, zenye joto na zilizotunzwa vizuri," na pia alisimamia mpango wenye thamani ya pauni milioni 670 wa kuboresha nyumba za umma (social housing).

Katika mahojiano yake ya kwanza na BBC tangu kuchaguliwa kwake, Abdi-Wali alisema: "Makazi ni tatizo kubwa hapa Camden, kote jijini London, na kote nchini. Hivyo, hili ni suala nitakalolifanyia kazi kila siku ili kuhakikisha tunaleta maboresho kwa ajili ya wananchi."