Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, unaopambana na waasi wa Kihouthi nchini Yemen, umetangaza kuwa ulifanikiwa kuzuia kuharibu kombora la cruise katika eneo la Madina, moja ya miji mitakatifu zaidi kwa waumini wa dini ya Kiislamu..

Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, alisema kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X: "Kombora la cruise lilikamatwa na kuharibiwa katika eneo la Madina."

Taarifa hiyo imeibua tahadhari kutokana na umuhimu wa kidini wa Madina, eneo ambalo Wahouthi waliwahi kusema hawatalilenga katika mashambulizi yao.

Huku hayo yakijiri Kundi la Wahouthi nchini Yemen limesema halikufanya shambulio lolote dhidi ya eneo la Madina siku ya Alhamisi, likikanusha madai yaliyotolewa na Saudi Arabia.

Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kutangaza kuwa ulikamata na kuharibu kombora lililokuwa likielekea eneo la mji mtakatifu wa Madina.

Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi, Yahya Saree, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba: "Vikosi vya ulinzi vya Yemen vinathibitisha kuwa havijafanya operesheni yoyote dhidi ya ardhi ya Saudi Arabia leo. Madai ya adui wa Saudi kwamba Madina ililengwa ni uongo mtupu na wa aibu."