WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba, amezitaka taasisi za ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) barani Afrika kuimarisha uaminifu, uwajibikaji na ubunifu ili kupanua huduma za kifedha, kuchochea uwekezaji na kuongeza fursa za ajira.


Akifungua Mkutano wa 26 wa SACCOS za Afrika jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 15,2026 Dk. Nchemba amesema vyama hivyo vina nafasi muhimu katika kukusanya akiba, kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara na kuharakisha mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.

Amesema mkutano huo unatoa fursa ya kujadili mustakabali wa mitaji, biashara na ajira za Waafrika, huku ukilenga kuimarisha mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo ya uchumi wa bara hilo.

“Tumekutana hapa kujadili mustakabali wa mitaji ya Afrika, biashara za Afrika, ajira za Waafrika na, hatimaye, mageuzi ya kiuchumi ya bara letu,” amesema Waziri Mkuu Dk.Mwigulu.

Amefafanua Tanzania inautazama mkutano huo kama jukwaa la kuunganisha mawazo, mitaji na biashara za Afrika na fursa za kimataifa, pamoja na kuwawezesha viongozi wa ushirika kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Ameongeza kaulimbiu ya mkutano huo, “Kujenga Uaminifu, Kuchochea Mageuzi: Mustakabali wa Ushirika wa Kifedha Barani Afrika,” inasisitiza umuhimu wa kuimarisha uaminifu na uwajibikaji ili kujenga taasisi za ushirika zilizo imara na endelevu.

“Bila uaminifu, ushirika hauwezi kuwepo, na bila mageuzi, hakuna mustakabali,” alisema.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu kwa washiriki wa mkutano huo na kuwataka kuendeleza taasisi zinazozingatia uaminifu, uwajibikaji, ubunifu na utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji ya wanachama.

Pia amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye amesisitiza mchango wa SACCOS katika kupanua huduma za kifedha, kuendeleza ujasiriamali, kuunda ajira na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Takwimu zilizowasilishwa katika mkutano huo zinaonesha kuwa hadi mwisho wa mwaka 2025, Tanzania ilikuwa na SACCOS 981 zilizosajiliwa, zenye wanachama na wanufaika wapatao milioni 1.9. Jumla ya mali za SACCOS hizo ilifikia Sh1.69 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.8.

Katika kipindi hicho, faida kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 24, mapato kwa asilimia 18 na mikopo kwa asilimia 17.

Hata hivyo, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 2.7 pekee, hali inayoonesha kuwa ukuaji wa shughuli za kifedha ulitokana zaidi na wanachama waliokuwepo kuendelea kuweka akiba na kukopa zaidi.

Awali kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo, amesema Tanzania ina historia ndefu ya ushirika, iliyoanzia kwa wakulima wa kahawa kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro walioungana kutafuta masoko ya mazao yao kabla ya uhuru.

Amesema SACCOS zina nafasi kubwa ya kufadhili sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na biashara, akizitaka kuandaa mifumo bunifu ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima kuwekeza katika pembejeo, teknolojia za kisasa, mitambo ya kilimo, uchakataji wa mazao na upatikanaji wa masoko.

Ameongeza Serikali inaendelea kuimarisha udhibiti na usimamizi wa vyama vya ushirika kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, huku ikiendeleza utawala bora na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Pia amesema Serikali inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika SACCOS kama wanachama na viongozi, huku mkutano huo ukitarajiwa kutoa mikakati ya kupanua mikopo yenye masharti nafuu na kuongeza mchango wa ushirika katika ukuaji wa uchumi.