Usafiri wa Mchungaji.
Usafiri wa Muumini.

Na Makongoro Oging' na Haruni Sanchawa
RIPOTI nzito inayohusu utajiri wa kutisha kwa baadhi ya viongozi wa dini wakiwemo wachungaji na maaskofu na kuweka utofauti mkubwa wa maisha baina ya waumini, umezua gumzo kubwa katika makanisa mbalimbali nchini.
Waumini wengi waliozungumza na gazeti hili wamewashitukia baadhi ya viongozi hao wa dini kutokana na kile walichodai kuwa wamezidi kujilimbikizia mali huku wakiwahimiza (waumini) kutoa sadaka na michango mbalimbali ya mara kwa mara.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya waumini wamekuwa wakihama kutoka kanisa moja kwenda lingine huku wakiamini kuwa Mungu atawasaidia wabadilike kimaisha au kumaliza matatizo yao.
Kutokana na mgongano huo baina ya viongozi wa makanisa na waumini, baadhi ya wachungaji na maaskofu waliozungumza na gazeti hili walikuwa na michango yao juu ya hali hiyo na walizungumza kama ifuatavyo:

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk. Valentino Mokiwa akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hilo la viongozi wa dini kujitajirisha alishauri kwamba makanisa ya watu binafsi ambayo viongozi wao wamejipatia mali nyingi zenye utata wachunguzwe kwa karibu.
“Viongozi wa dini au muumini kuwa tajiri siyo jambo baya kwani hata sisi katika makanisa yetu ya Anglikana kuna maaskofu matajiri na maskini na hakuna sheria inayomkataza kiongozi wa dini kuwa tajiri bali inategemea jinsi alivyoupata, ambao haijulikani utajiri wao umetoka wapi, wachunguzwe,” alisema Askofu Mokiwa.


Aliongeza kuwa utajiri huo wa viongozi wa dini inabidi uwe ameupata kihalali, vinginevyo itakuwa ni dhambi kwa Mungu.
Alisema kwamba utajiri wa viongozi unaweza kutokana utafutaji kwa njia ya halali alitolea mfano wakati anasomea uchungaji nchini Marekani, kwamba walikuwa wakifundishwa ujasiriamali wa kupata fedha kwa njia ya kilimo.

Naye Mchungaji Christopher Mtikila alisema kwamba viongozi wa dini kujitajirisha na kuwasahau waumini wao au kutumia fedha za waumini maskini kujineemesha hao hawana wito wa Mungu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe alisema viongozi wa dini na hata wasio viongozi wanapaswa kujiwekea utajiri mbinguni na si duniani.
Askofu Kakobe ambaye amesifiwa na watu wengi kwa kuonesha kwenye televisheni nyumba na hata chumba chake cha kulala na kutajwa kuwa ni mfano, alisema kwake yeye anachokifanya ni kufundisha watu kuwekeza mbinguni.
“Siwezi kuacha kukemea watu wanaovaa vimini, wigi, kusuka nywele bandia, kuvuta sigara eti kwa sababu tutakosa sadaka,…kipaumbele ni Mungu,” alisema Askofu Kakobe.

Nabii Flora
Nabii Flora wa Kanisa la Maombezi lililoko Mbezi Beach kwa upande wake alisema mtumishi wa Mungu aliye wa kweli hawezi kutajirika huku waumini wake wanalia na shida.
“Kanisa ni sehemu ya jamii ambayo inasaidia watu mbalimbali kupata Neno la Mungu pamoja na kusaidia shida za kijamii, si sehemu ya kiongozi kujitajirisha,” alisema.

Mch. Mtemela
Naye Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste jijini, Alphonce Mtemela amesema kwamba katika Kitabu cha Biblia Yohana 3.1 Mungu amesema utakuwa mbunifu kuwasaidia watu wako unawaongoza ili wafurahie wokovu wa Mungu.
“Kutokana na kifungu hicho ni wazi Mungu hataki mtu aishi maisha ya majuto au masikitiko baada ya kumjua yeye.”
Akaongeza kwamba wokovu siyo mzigo ni furaha na kiongozi hapaswi kufurahi kuona watu anaowaongoza maisha yao yakiwa ni ya majuto wakati yeye anaishi maisha mazuri.
Alisema watumishi wa Mungu waangalie jinsi ya kuwasaidia watu wenye shida na siyo waishie kubadili suti na kujitajirisha kila siku wakati waumini wanateseka na kuishi maisha ya shida.
Mch. Rwakatare
Hata hivyo, Mchungaji Getruda Rwakatale kwa upande wake alipohojiwa hakupenda kuchangia lolote kuhusiana na suala hilo.Waumini wanasemaje
Uwazi liliongea na baadhi ya waumini wa madhehebu kadhaa kwa nyakati tofauti walisema mtumishi wa Mungu wa kweli ni yule anayejali maisha ya waumini wake na siyo yule anayejilimbikizia mali huku ‘kondoo’ wake wakitaabika.
Mmoja wa waumini hao alisema anapeleka sadaka kanisani ambayo inamzidi uwezo, kitu ambacho si sahihi hata kwa Mungu.
Furaha Josephat ambaye amewahi kuwa muumini wa Kanisa la Efatha na sasa anasali Kanisa la Romani Katoliki, Mwenge amesema kwamba wachungaji wanakosea wanapokuwa matajiri.
“Haiwasaidii, ni bora mali zikiwa nyingi zitolewe kwa wasiojiweza pamoja na yatima kama sadaka,” alishauri Josephat.
Aliongeza kwamba viongozi wengi wa dini wanapenda kujilimbikizia mali bila kutoa msaada, akawashauri waangalie maeneo mbalimbali ya kutoa msaada kama vile kujenga hospitali, shule na visima vya maji.
Naye Mary Andemile ambaye alijitambulisha kuwa huwa anasali Kanisa la Gwajima alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa wawasaidie watu wenye hali duni badala ya kujitajirisha.
Alitoa mfano kuwa Mchungaji Gwajima
ni kiongozi ambaye siyo tajiri lakini amekuwa akiwasaidia waumini wake jinsi ya kujikwamua na maisha magumu.
Muumini mwingine, Francis Mbena kwa upande wake aliwashauri viongozi wa dini wasiwafanye waumini wao kuwa vyanzo vyao vya mapato ili wawe matajiri.
“Ni vema mtu akatoa sadaka kulingana na uwezo wake, wasitumie imani kuwalazimisha waumini kutoa michango mingi huku wakijua hali zao ni duni, huko ni kuwanyonya,” alisema.
Daudi Antony kwa upande wake amesema kuwa ukweli ni kwamba kutokana na utajiri wa viongozi kuwa mkubwa, wakiwemo wanasiasa, taifa linaelekea kugawanyika.
“Makanisani, serikalini sasa hakuna huduma, baadhi ya wachungaji wamegeuza makanisa kama miradi yao vivyo hivyo kwa viongozi wa serikali, ofisi zao ni miradi ya kuchumia fedha au ni biashara,” alisema Anthony.
Naye Gerad Philipo amesema viongozi wengi wa dini wameshindwa kuwa na huruma kwa watu wanaowaongoza kwani huwakamua na hasa ile kanuni ya fungu la kumi, alidai inaumiza wale wasiokuwanacho.