Musa Mateja na Shakoor Jongo
KUNDI la wachekeshaji la Orijino Komedi linaloundwa na mastaa, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Lucas Mhuvile ‘Joti’, Joseph Shamba ‘Vengu’, Slivery Mujuni ‘Mpoki’, Alex Chalamila ‘MacRegan’ na Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’ chini ya Sekioni David ‘Seki’, linadaiwa kwisha huku kila mmoja akijiingiza katika fani nyingine ili kujipatia mkate wa siku.

UPEKUZI WA IJUMAA WIKIENDA WABAINI SIRI NZITO
Kwa muda mrefu sasa, Ijumaa Wikienda limekuwa likipokea malalamiko ya mashabiki wa mastaa kuwa michezo yao mipya haionekani kama zamani huku wakidaiwa kurudiarudia ya zamani.
Kwa mujibu wa vyanzo makini vilivyozungumza na gazeti hili, kundi hilo linaloruka hewani kupitia Runinga ya TBC 1, linadaiwa lilimaliza mkataba wake tangu Januari Mosi, mwaka huu na kusitisha uandaaji wa vipindi vipya.

INASIKITISHA
Ilidaiwa kuwa vijana hao watafutaji wamekuwa kwenye wakati mgumu kimaisha kwani walitarajia kulamba mkataba mpya hivyo baada ya kuona kimya, kila mmoja akaanza kusaka ‘ngawira’ katika fani nyingine.
 MASANJA
Ilielezwa kwamba Masanja amejikita kwenye muziki wa Injili akiwa kwenye ‘tizi’ la uchungaji, utangazaji na ushereheshaji.

MPOKI
Kama ilivyo kwa Masanja, pamoja na kwamba alianza muziki wa Kizazi Kipya akiwa bado anachekesha kideoni, Mpoki sasa amejikita katika Bongo Fleva na utangazaji huku akiuza nyago kwenye video za wasanii wa muziki Bongo.

VENGU
Kwa upande wake Vengu yuko kwenye matibabu nchini India baada ya kusumbuliwa na maumivu sehemu ya kichwa kwa muda mrefu.

JOTI
Joti kwa sasa anajihusisha

na muziki wa kizazi kipya huku kukiwa na taarifa kwamba pia amekuwa akilamba dili za ushereheshaji.

WAKUVWANGA NA MACREGAN
Jamaa hao wakali wa kuchekesha walidaiwa kuwa kwa sasa hawaonekani kideoni lakini wamekuwa wakilamba shavu kwenye shughuli za ushereheshaji.

NDIYO MWISHO WA KUVUNJA WATU MBAVU?
Ilielezwa kuwa kuonekana kwao wakijishughulisha na mambo mengine bila kurekodi vipindi vipya, inawezekana ndiyo mwisho wa kuvunja watu mbavu.
Ijumaa Wikienda limekuwa likizungumza na mastaa hao kujua kulikoni, lakini wamekuwa wakirusha mzigo kwa Seki kuwa ndiye mwenye ‘a na be’ ya hatima ya kundi hilo hivyo aulizwe yeye.
Akizungumzia ishu hiyo, meneja wa programu hiyo wa TBC1, Mwanga Slay alikuwa na haya ya kusema:
“Kwa taarifa kamili ni vizuri mkazungumza na Seki kwa sababu yeye ndiye anayeweza kulizungumzia.”

SEKI VIPI?
Juhudi za kumpata Seki hazikuzaa matunda baada ya simu yake kutokupokelewa kila ilipopigwa hivyo bado zinaendelea.