MWENYEKITI wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba, Jaji Joseph Warioba amevitaka vikundi na wananchi waliopendekeza wajumbe wa Tume hiyo, kuiacha ifanye kazi iliyopewa kufanya.
Pamoja na hayo, Tume hiyo jana ilikabidhiwa rasmi jengo la ofisi ya kufanyia kazi, kuahidiwa magari 30, kuajiri watumishi wa sekretarieti watakaosaidia na kuanzishiwa fungu maalumu la kuiwezesha kufanya kazi.
Akizungumza wakati Tume hiyo inakabidhiwa ofisi Dar es Salaam, Jaji Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, alisema waliopendekeza majina ya wajumbe hao, wasitarajie kuwa wajumbe hao watafanya watakavyo wao kwani Tume hiyo ni ya Watanzania wote na si watu wachache.
“Naomba kwa dhati kabisa, waliotupendekeza watuache tufanye kazi, tumepewa jukumu la nchi tuacheni tufanye kazi bila shinikizo,” alisema Jaji Warioba.
Alisema iwapo waliopendekeza Tume hiyo wanadhani kuwa wameweka watu wao hivyo mambo yatafanyika kama wanavyotaka wao, watakuwa wanajidanganya kwa kuwa kazi ya Tume ni moja tu ya kutumikia wananchi.
Alisema majukumu ya Tume hiyo si kuandika Katiba bali kukusanya maoni, kuyachambua na kuandika rasimu ya Katiba ambayo itazaa Katiba mpya.
Alihamasisha wananchi kujiandaa na kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Alisema Tume hiyo iliyoanza kazi juzi, inaandaa utaratibu utakaoiwezesha kufikia wananchi wengi ili kupata maoni mengi.
“Sisi Tume tunatarajia Watanzania watatwambia wanataka Tanzania iweje katika Katiba,” alisema. Aliziomba Serikali za Mitaa kuanzia vijiji, tarafa, kata, wilaya na mikoa, kujiandaa kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa Tume hiyo kufikia wananchi wengi zaidi.
Awali akimkabidhi funguo za jengo hilo la ghorofa 10 kuwa ofisi ya Tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema pamoja na jengo hilo, pia kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Tume hiyo itapewa magari 30 ili kuiwezesha kiusafiri.
Usalama wao Alisema Serikali pia imeandaa ulinzi wa kutosha utakaotumia mitambo maalumu katika jengo hilo, ili kuwahakikishia wajumbe usalama wao, kuwawekea vifaa vya kisasa vya kukusanyia na kutunza kumbukumbu na kuwafungulia tovuti rasmi ya Tume.
Pia alisema Serikali imejiandaa kuongeza sekretarieti yenye utaalamu, ili kufanikisha kazi zake ambayo katika eneo la makazi, wajumbe wote ambao hawaishi Dar es Salaam, watapewa nyumba mpya zenye samani wakati wote watakaokuwa wanafanya kazi za Tume.
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, aliitaka Tume kujipanga kutoa elimu kuhusu Katiba ya sasa, ili kuwapa welewa wananchi kuhusu Katiba hiyo ambapo pia Wizara yake itaendelea kutoa elimu hiyo.
Alisema Tume imepewa kazi nzito isiyohitaji ubaguzi wa aina yoyote ambayo inahitaji uaminifu, nguvu, maarifa na uvumilivu. “Najua mtalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu usiku na mchana, ila tambueni kuwa Serikali iko pamoja nanyi,” alisema Balozi Sefue.
Wajumbe Wajumbe 30 wa Tume hiyo pamoja na Jaji Warioba ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu mstaafu Augustine Ramadhani, Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Mngwali, Dk. Sengondo Mvungi, Jesca Mkuchu na Alhaji Said El-Maamry.
Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Al-Shaymaa Kwegry, Richard Lyimo, John Nkolo, Mwantumu Malale na Joseph Butiku.
Kutoka Zanzibar ni Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohamed, Simai Mohamed Said na Muhammed Yussuf Mshamba.
Wengine ni Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohamed Ali, Ally Abdullah Saleh na wajumbe wa Sekretarieti ni Assa Ahmad Rashid ambaye ni Katibu na msaidizi wake, Casmir Kyuki. Tume itafanya kazi kwa miezi 18.
0 Comments