Wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Mahakama moja ya rufaa nchini Cameroon, imefutilia
mbali hukumu dhidi ya watu wawili waliofungwa jela mwaka wa 2011, baada
ya kupatikana na hatia ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja.
Wakili wawili Alice Nkom , amesema amefurahishwa
na uamuzi huo kwa sababu jaji aliyetoa hukumu dhidi yao, alifanya hivyo
chini ya shinikizo ya watu fulani.
Mapenzi ya jinsia moja imeharimishwa nchini humo.
Novemba mwaka wa 2011, mahakama iliwapata na
hatia wawili hao na kuwahukumu kifungo cha miaka mitano gerezani, baada
ya polisi kuwakamata wakifanya ngono katika gari moja mjini Yaunde.
Wawili hao walikana mashtaka hayo.
Lakini mapema hii leo mahakama hiyo ya rufaa iliagiza kuwa washukiwa hao hawakuwa na kosa lolote.
Akizungumza na BBC Bi Nkom alisema kuwa uamuzi huo sio wa kushangaza.
''Wateja wangu hawakuwa wakifanya lolote wakati walipokamatwa na polisi'' Alisema Bi Nkom.
Kwa kuwa walikuwa wamevalia nguo za wanawake na
kujipaka vipodozi, polisi walisema kuwa wao ni wanachama wa mtandao
mmoja unaohimiza mapenzi ya jinsia moja''
Hata hivyo amesema, upande wa mashtaka haujaelezea ikiwa utawasilisha rufaa kupinga uamuzi huo wa mahakama ya juu zaidi.
Wanaume hao wawili wanatarajiwa kuachiliwa siku ya Jumanne.
Shirika la kimataifa linalotetea maslahi ya wapenzi wa jinsia moja, limepongeza uamuzi huo.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Andre Banks,
amesema ni dhihirisho kuwa mahakama zinaweza kutekeleza majukumu yake
kwa njia ya haki na usawa.
Bi Nkom, vile vile ameiambia BBC kuwa mwezi
uliopita, mahakama hiyo ya rufaa, iliidhinisha hukumu ya kifungo cha
miaka mitatu gerezani dhidi ya raia mwingine wa Cameroon, Roger
Jean-Claude Mbede, chini ya sheria za kupambana na mapenzi ya jinsia
moja. |
1 Comments